Wanajeshi wawili wa Uganda wahukumiwa adhabu ya kifo kwa kuwaua raia nchini Somalia
2021-11-15 09:12:56| CRI

Wanajeshi wawili wa Uganda wanaotuhumiwa kuwaua raia saba wa Somalia mwezi Agosti wakiwa wanafanyakazi chini ya tume ya kulinda amani ya Umoja wa Afrika (AMISOM) wamehukumiwa kifo huku wengine watatu watafungwa miaka 39 jela baada ya kupatikana na hatia kwenye mahakama ya kijeshi.

AMISOM imesema Mahakama ya Kijeshi iliyoanza kusikiliza kesi tarehe 1 hadi 12 mwezi Novemba katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, ilipitia taarifa zote zikiwemo za mashahidi na kuwapata wanajeshi hao na hatia ya kuwaua raia huko Goloweyn mnamo tarehe 10 mwezi Agosti.

Tume hiyo imesema katika taarifa kwamba watano hao watarejeshwa nchini kwao Uganda kutumikia vifungo vyao.

Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda ambaye pia ni Kamanda wa Kombania ya 1 ya AMISOM Bw. Don Nabasa amesema kama askari, wana jukumu la kulinda maisha na mali, na kazi yao nchini Somalia ni kudhoofisha kundi la al-Shabab na vikundi vingine vyenye silaha, na hili liko wazi kabisa kwenye Kanuni za Ushirikiano.