Maonyesho ya Biashara Afrika yaanza Afrika Kusini
2021-11-16 09:40:58| CRI

Maonyesho ya Biashara Afrika IATF yameanza mjini Durban, Afrika Kusini yakiwa na wito wa kuwataka Waafrika kubadilishana mawazo ili kuboresha biashara barani humo.

Akihutubua ufunguzi wa maonyesho hayo, rais wa zamani wa Nigeria na mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la IATF kwa mwaka 2021 Olusegun Obasanjo alisema maonyesho hayo ya biashara yanaweza kutoa fursa kwa washiriki kutangaza bidhaa na huduma, kubadilishana mawazo ya biashara na kufikia makubaliano. Alisema IATF pia inaweza kuchukuliwa kama jukwaa la kujadili biashara kwa Waafrika na kutekeleza Eneo la Biashara Huria la Afrika AfCFTA.

Obasanjo alieleza matumaini yake kuwa maonyesho hayo ya biashara yataweza kushughulikia changamoto zinazoathiri biashara barani Afrika ambazo ni pamoja na vizuizi mpakani.

Katibu Mkuu wa sektretarieti ya makubaliano ya AfCFTA Wamkele Mene alisema makubaliano hayo yana malengo mazuri kama kuwaondoa watu milioni 100 kwenye umaskini uliokithiri kabla ya mwaka 2035 na kuongeza biashara barani Afrika.