Afrika Mashariki yahimizwa kuharakisha mapitio ya ushuru wa forodha wa pamoja ili kuhimiza biashara
2021-11-16 09:37:57| CRI

Nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC zimehimizwa kuharakisha mapitio ya kina ya ushuru wa forodha wa pamoja wa Afrika Masharaki (CET) ili kuhimiza biashara na ukuaji wa viwanda katika kanda hii.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo, Mwenyekiti wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Afrika Mashariki (SCITFI) Betty Maina amesema kushindwa kukamilisha mapitio ya CET, ambayo yameanza mwaka 2016, kunatoa uhuru kwa bidhaa kutoka sehemu nyingine duniani kufurika kwenye soko la pamoja la Afrika Mashariki kwa gharama za kanda hiyo.

Akiongea kwenye ufunguzi wa kikao cha 39 cha mawaziri wa SCITFI, Maina ambaye pia ni Waziri wa Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Makampuni wa Kenya, amesema kukamilika kwa mapitio hayo kutawezesha kanda hiyo kufanya biashara zaidi, pamoja na kuhimiza ukuaji wa viwanda vya Afrika Mashariki.