UM, IGAD yaonya hali ya ukame kuwa mbaya zaidi katika pembe ya Afrika
2021-11-19 10:45:14| CRI

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Maendeleo ya Kiserikali la nchi za Afrika Mashariki (IGAD) yametahadharisha kuwa hali ya ukame itazidi kuwa mbaya, na ukosefu wa chakula huenda ukaongezeka katika nusu ya kwanza ya mwaka 2022 katika pembe yote ya Afrika.

Kwenye taarifa yao, Katibu Mtendaji wa IGAD Wokneh Gebeyehu na Mratibu wa kanda ndogo ya Afrika Mashariki wa FAO Chimimba David Phiri wametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kupunguza athari za ukame katika kanda hiyo, zikiwemo kulinda maisha ya watu, kuokoa maisha na kuzuia uwezekano wa kutokea baa la njaa katika baadhi ya maeneo.

Kwa mujibu wa Kundi linaloshughulikia Usalama wa Chakula na Lishe linaloongozwa na IGAD na FAO, hadi kufikia Oktoba, watu milioni 26 tayari wameshaathirika na ukosefu mkubwa wa chakula, ambapo jamii zilizoko kwenye hatari zaidi za kanda ya IGAD ni pamoja na Kenya, Djibout, Ethiopia na Sudan, ambazo sasa zinaendelea kushuhudia athari mbaya ambazo zimepelekea ukosefu wa chakula na lishe.