China yataka Lithuania irekebishe makosa yake mara moja
2021-11-23 09:01:45| cri

China yataka Lithuania irekebishe makosa yake mara moja_fororder_立陶宛

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Zhao Lijian amesema uamuzi wa Lithuania kuiruhusu Taiwan kufungua eti ofisi ya mwakilishi nchini humo umeenda kinyume na ahadi ya kisiasa iliyotolewa na nchi hiyo ilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Jamhuri ya Watu wa China, na kuongeza kuwa serikali ya Lithuania inatakiwa kuwajibika na matokeo yote mabaya na kurekebisha makosa yake mara moja.

Msemaji Zhao amesema hayo akizungumzia taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Lithuania kuwa inasikitishwa na uamuzi wa China wa kushusha ngazi ya uhusiano wa kidiplomasia na Lithuania kuwa ya kaimu balozi (charge d'affaires). Bw. Zhao amesema hatua hii ya Lithuania imejenga taswira potofu ya kuwepo kwa “China moja, Taiwan moja” duniani na kutoa mfano mbaya.

Bw. Zhao pia amesema Lithuania kubisha kuwa ofisi hiyo ya mwakilishi haina hadhi ya kidiplomasia ni uwongo, na kwamba mamlaka za Taiwan kudai kuwa kuanzishwa kwa “Ofisi ya Mwakilishi ya Taiwan” nchini Lithuania ni “hatua kubwa ya kidiplomasia” iliyopigwa na Taiwan, ni kujitangaza kidhahiri kwa mamlaka za Taiwan na watu wanaotaka “uhuru wa Taiwan”, na pia ni ushahidi kamili wa vitendo vyao wa kutafuta “uhuru wa Taiwan”.