Rada mpya katika uwanja wa ndege wa Mwanza kuimarisha usafirishaji wa samaki nje ya nchi kwa njia ya ndege
2021-11-25 08:52:10| CRI

Rada mpya ya kisasa iliyowekwa kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza karibu na Ziwa Victoria nchini Tanzania, inatarajiwa kuimarisha usalama na huduma za safari za ndege mkoani Mwanza, na kuinua usafirishaji wa samaki kwenda nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania Bw. Hamza Johari amesema ana matumaini kuwa rada hiyo pamoja na kuwepo kwa jengo la jokofu la kisasa kwenye uwanja wa ndege vitasaidia kuongeza usafirishaji wa samaki kwenda kwenye masoko ya Ulaya. Bw. Johari amesema Tanzania imekuwa ikisafirisha samaki wake kwenda Ulaya kupitia Kenya na Uganda, kutokana na changamoto za usalama kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza.

Mwezi Mei mwaka jana ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia ilisafirisha kwa mara ya kwanza zaidi kilo elfu 17 za samaki kutoka Mwanza, kwenda kwenye masoko ya Ubelgiji, Ujerumani, Ufaransa na Ureno.