Ushawishi wa China barani Afrika watokana na ushirikiano wa dhati kati ya pande hizo mbili
2021-11-25 16:05:20| cri

Ushawishi wa China barani Afrika watokana na ushirikiano wa dhati kati ya pande hizo mbili_fororder_pap-r8-china-34-countries-external_influence

Hivi karibuni, shirika maarufu la uchunguzi wa maoni la Afrika la Afrobarometer limetoa ripoti ya uchunguzi wa maoni, ikionesha kuwa ushawishi wa China barani Afrika unashika nafasi ya kwanza duniani, mbele ya Marekani, mashirika ya kikanda, mashirika ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika. Haya ni matokeo ya ushirikiano wa dhati kati ya China na Afrika kwa miaka mingi.

Uchunguzi huo uliofanywa katika nchi 34 barani Afrika unaonesha kuwa, kati ya watu 48,084 waliohojiwa ana kwa ana, asilimia 63 wanaona kuwa ushawishi wa China kwenye mambo ya uchumi na siasa katika nchi zao ulikuwa “mkubwa sana” au “mkubwa kwa kiasi”, huku asilimia 66 wakiamini kuwa ushawishi wa kiuchumi wa China barani Afrika ni chanya.

Kwa muda mrefu, China imekuwa ikifanya ushirikiano mzuri na nchi za Afrika katika nyanja mbalimbali, na kupata mafanikio mengi makubwa. Kwa upande wa biashara, China imeendelea kuwa mwenzi mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika kwa miaka 12 mfululizo. Tangu kuanzishwa kwa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), thamani ya biashara kati ya pande hizo mbili imeongezeka kuwa dola bilioni 200 za Kimarekani mwaka 2020 kutoka dola bilioni 10 ya mwaka 2000, na kuongezeka kwa mara 20. Kwa upande wa miundombinu, Afrika imekuwa soko la pili la China kwa miradi ya ujenzi wa miundombinu katika nchi za nje. China imetekeleza miradi mingi ya miundombinu kufuatia mahitaji ya nchi za Afrika. Takwimu zinaonyesha kuwa tangu kuanzishwa kwa FOCAC, makampuni ya China yameongeza na kuboresha zaidi ya kilomita 10,000 za reli na karibu kilomita 100,000 za barabara barani Afrika, na kutoa nafasi za ajira zaidi ya milioni 4.5. Kwa upande wa uwekezaji, uwekezaji wa moja kwa moja wa China barani Afrika umezidi dola bilioni 43.4, za kimarekani, na kushika nafasi ya nne kwa ukubwa wa uwekezaji barani Afrika. Matokeo haya ya ushirikiano yamezifanya China na nchi za Afrika kuwa washirika wa maendeleo wenye hatima moja.

Tangu kutokea kwa janga la COVID-19 barani Afrika, China imetoa misaada mbalimbali kwa nchi za bara hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa dawa na vifaa vya kujikinga na virusi, kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao, kutuma vikundi vya wataalam wa afya, na kutoa chanjo. Aidha, ili kuisaidia Afrika kukabiliana na athari za janga hilo kwa uchumi na jamii, China pia imefikia makubaliano ya kupunguza na kuahirisha malipo ya madeni na baadhi ya nchi za Afrika.

China ni rafiki na mshirika wa kutegemeka wa maendeleo wa Afrika. Ushirikiano wa China na Afrika unazingatia ustawi wa watu wa Afrika, na kufuata mahitaji na maslahi ya upande wa Afrika, bila ya kuweka masharti yoyote ya kisiasa. China inatumai kwa dhati kwamba nchi za Afrika zinaweza kujiendeleza na kujitegemea, na inapenda kuzisaidia nchi za Afrika katika kuongeza uwezo wao wa kujiendeleza. Hili linatambuliwa na kuthaminiwa na serikali na watu wa nchi za Afrika.

Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa FOCAC hivi karibuni utafanyika nchini Senegal. China na Afrika zitachukua fursa hii kupanua na kuimarisha zaidi ushirikiano wao katika nyanja mbalimbali, na kuendeleza ujenzi wa jumuiya ya China na Afrika yenye hatma ya pamoja.