WHO yatafuta mkataba wa janga kufuatia wasiwasi wa kirusi cha Omicron
2021-11-30 08:38:21| CRI

Kikao maalum cha Mkutano wa Afya Duniani (WHA) kimeanza jana, huku wasiwasi ukiongezeka kutokana na virusi vya Corona vilivyobadilika vya Omicron, na washiriki wakijadiliana mkataba mpya wa kukabiliana na janga hilo.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dr. Tedros Ghebreyesus amesema, janga la COVID-19 limeweka wazi udhaifu uliopo katika mfumo wa maandalizi na majibu ya majanga duniani. Amesema njia nzuri ya kukabiliana na majanga hayo ni kwa kupitia makubaliano ya kisheria kati ya mataifa, makubaliano yanayotokana na kutambua kwamba, hakuna hatma isipokuwa hatma ya pamoja.

Ingawa WHO imesema bado haiko wazi kama virusi vya Omicron vinaambukiza zaidi ama vina dalili kali zaidi kuliko virusi vya aina nyingine ikiwemo Delta, wasiwasi umeongezeka juu ya athari yake kwa chanjo za COVID-19 zilizopo sasa pamoja na matibabu.