Ugonjwa wa UKIMWI bado umebaki kuwa tatizo kubwa ambalo linaathiri afya ya mamilioni ya watu duniani. Ingawa dunia imepiga hatua kubwa katika miongo ya hivi karibuni, lakini malengo muhimu ya mwaka 2020 duniani bado hayajatimizwa. Masuala ya mgawanyiko, ubaguzi na kutozingatiwa kwa haki za binadamu ni miongoni mwa sababu zinazofanya UKIMWI kuendelea kuwa janga la afya duniani. Hivyo kila ifikapo Disemba 1, viongozi na watu wa kawaida huwa wanakumbushana juu ya madhila ya janga hili pamoja na kukabiliana na hali ya kutokuwepo kwa usawa katika kupambana na UKIMWI, vilevile kufikia watu ambao hadi sasa bado hawajapatiwa huduma za lazima za UKIMWI. Kaulimbiu ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka huu ni "Komesha ukosefu wa usawa, komesha UKIMWI, komesha janga la virusi".