Kenya yasema kasi ya maambukizi mapya ya VVU yaendelea kupungua
2021-12-02 08:52:27| CRI

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema katika miaka ya hivi karibuni Kenya imepata maendeleo makubwa katika kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi vya UKIMWI. Rais Kenyatta amesema hayo jana kwenye maadhimisho ya siku ya kupambana na Ukimwi Duniani, wakati idadi ya maambukizi mapya nchini Kenya ikipungua kwa asilimia 68.4 kati ya 2013 na 2021.

Rais Uhuru Kenyatta pia amesema mwaka huu vifo vinavyotokana na ugonjwa wa UKIMWI nchini Kenya vimepungua kwa asilimia 67 hadi kufikia 19,486, kutoka vifo 58,446 mwaka 2013. Pia kumekuwa na ongezeko la asilimia 83 ya watu wanaotumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi kutoka watu laki 6.5 wa mwaka 2013 hadi watu milioni 1.19 wa mwaka huu. Amesema mafaniko hayo yanatokana na uwekezaji unaoongezeka wa serikali katika upimaji, uzuiaji na udhibiti wa UKIMWI na magonjwa nyemelezi.

Hata hivyo amesema kuna hali ya kusikitisha kuwa watu walio hatarini zaidi katika jamii hasa maskini, waliotengwa, watoto, wanawake, vijana ndio wanaathiriwa zaidi ya ugonjwa huo.