Rwanda yataka kuimarisha ushirikiano na China katika elimu ya uvumbuzi wa teknolojia
2021-12-03 08:46:06| CRI

Waziri wa Elimu wa Rwanda Bibi Valentine Uwamariya amesema Rwanda inatafuta ushirikiano zaidi wa kisayansi na kiteknolojia na China ili kuchochea ukuaji wa uvumbuzi na elimu ya utafiti.

Akiongea na wanahabari mjini Kigali kwenye Kongamano la 13 la majadiliano ya sera la kikosi kazi cha Kimataifa kuhusu walimu, Bibi Uwamariya amesema anafahamu kuwa China ina viwanda tofauti ambapo mifano ya kazi zinazofanywa na wanafunzi na watafiti zinaweza kuletwa katika ngazi nyingine na kufanyiwa biashara.

Amesema ushirikiano kwenye sekta ya elimu kati ya China na Rwanda umetoa fursa kwa wanafunzi wa Rwanda kupata masomo zaidi nchini China kwenye kozi za teknolojia kama vile za uhandisi na teknolojia ya habari na mawasiliano.

Bibi Uwamariya ameishukuru serikali ya China kwa kushirikiana na Rwanda kujenga chuo cha kisasa cha VETA katika wilaya ya Musanze, Mkoa wa kaskazini. Amesema wanaojiunga na chuo hicho wanaendana na dira na dhamira ya serikali ya kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya elimu ya ufundi stadi.