China na Sierra Leone zaahidi kuimarisha ushirikiano
2021-12-07 09:38:19| cri

Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio amekutana na mwanadiplomasia mwandamizi wa China Bw. Yang Jiechi, ambapo pande hizo mbili zimeahidi kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

Kwenye mkutano huo, Bw. Yang amewasilisha salamu za dhati za Rais Xi Jinping wa China kwa rais Bio. Amesema marais hao wawili wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu na kupeana salamu za pongezi kwa maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Sierra Leone, na kufikia makubaliano muhimu kuhusu kuimarisha uaminifu wa kisiasa na kuzidisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

Bw. Yang ameongeza kuwa China inapenda kushirikiana na Sierra Leone kutekeleza mipango ya FOCAC, kuratibu makubaliano ya mkutano huo juu ya matakwa ya maendeleo ya Sierra Leone, na kuongeza zaidi ushirikiano katika nyanja zikiwemo mapambano dhidi ya janga, kilimo, uvuvi, elimu na miundombinu, kuisaidia Sierra Leone kupambana na janga hili na kufufua uchumi wake.

Kwa upande wake, rais Bio alimtaka Yang kuwasilisha salamu zake za heri kwa rais Xi na kutoa pongezi za dhati kwa mafanikio ya kikao cha sita cha Kamati Kuu ya 19 ya CPC. Rais Bio amesema China imetoa mchango mkubwa kwa amani na maendeleo ya dunia na kuwa mfano kwa nchi zinazoendelea. Ameongeza kuwa Sierra Leone inashikilia kithabiti kanuni ya kuwepo kwa China moja na inaunga mkono Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing 2022.