Marekani yasema haitawaadhibu wanajeshi wake kutokana na shambulizi lililosababisha vifo vya raia 10 Kabul
2021-12-14 09:11:51| CRI

Wizara ya ulinzi ya Marekani imesema wanajeshi waliohusika na shambulizi lililosababisha vifo vya raia 10 wakiwemo watoto 7 huko Kabul, mji mkuu wa Afghanistan mwezi wa Agosti hawatakabiliwa na adhabu.

Msemaji wa wizara hiyo Bw. John Kirby amewaambia wanahabari kwamba waziri wa ulinzi Bw. Lloyd Austin ameidhinisha mapendekezo kutoka kwa mkuu wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani Jenerali Keneth McKenzie na mkuu wa Kamandi ya Operesheni Maalumu ya Marekani Jenerali Richard Clarke, kutowachukulia hatua yoyote waliohusika na shambulizi hilo lililotokea Agosti 29.

Wizara hiyo mwezi wa Septemba ilitambua kuwa shambulizi la droni lililofanywa katika siku za mwisho wakati jeshi la Marekani likiondoka Afghanistan, lilikuwa kosa la kusikitisha ambalo lilisababisha vifo vya raia wa kawaida wakiwemo watoto 7.

Kabla ya hapo, maofisa wa wizara hiyo walisema, shambulizi hilo lilikuwa la lazima ili kuzuia tishio la kundi la ISIS-K dhidi ya vikosi vya Marekani vilivyokuwa vikiwahamisha watu katika uwanja wa ndege wa Kabul.