Mkutano kuhusu afya ya umma barani Afrika wafunguliwa Nairobi
2021-12-15 09:19:29| CRI

Mkutano wa kwanza kuhusu masuala ya afya ya umma barani Afrika (CPHIA 2021) ulifunguliwa Jumanne ambapo viongozi, watunga sera na wanasayansi wametoa wito wa kuimarishwa mwitikio wa janga la virusi vya Corona kufuatia kugunduliwa kwa virusi vipya vilivyobadilika.

Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema mabadiliko yanatakiwa kufanywa kwenye mifumo ya afya ya umma wa Afrika, ili kuimarisha mwitikio wa bara hilo kwa janga la Corona ambalo limetoa pigo kubwa kwa uchumi na maisha ya watu.

Kwa mujibu wa rais Kagame, janga hilo lenyewe ni kama wito kwa Afrika kuwekeza kwenye mifumo ya afya yenye ustahimilivu, kuongeza uzalishaji wa chanjo, dawa na vitendanishi, na kuboresha uwezo wa wahudumu wa afya.

Habari nyingine zinasema, Kamisheni ya Umoja wa Afrika siku hiyo imesema, janga la Corona linaloendelea linatoa fursa ya kihistoria kujenga utaratibu mpya wa afya ya umma barani Afrika ili kukabiliana na misukosuko ya afya inayoweza kutokea katika siku zijazo.