China itajibu kithabiti endapo Marekani itapitisha muswada wa sheria unaohusiana na suala la Xinjiang
2021-12-16 09:06:40| CRI

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bw. Zhao Lijian amesema, China inapinga kithabiti bunge la Marekani kuingilia mambo ya ndani ya China kupitia suala la Xinjiang, na itajibu kithabiti endapo Marekani itaendelea kusukuma mbele muswada husika.

Bw. Zhao Lijian amesema hayo kufuatia Baraza la Chini la Bunge la Marekani kupitisha muswada wa kuzuia utumikishwaji wa watu wa kabila la Wauigur, na kupanga kuuwasilisha kwa rais usainiwe baada ya kupitishwa na Baraza la Seneti.

Msemaji huyo amesema baadhi ya wanasiasa wa Marekani wanasambaza uvumi na kupotosha ukweli kuhusu suala la Xinjiang, kucheza mchezo wa siasa na kufanya umwamba wa kiuchumi kwa kisingizio cha haki za binadamu, wakijaribu kukwamisha maendeleo ya China kwa kutumia suala la Xinjiang. Bw. Zhao amesema kamwe njama yao haitafanikiwa, watakachofanikiwa tu ni kuharibu zaidi sifa na sura ya Marekani nchini China.