Maafisa wa Marekani waomba viza ya kuhudhuria Michezo ya Olimpiki ya Baridi ya Beijing
2021-12-28 09:45:11| CRI

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Zhao Lijian amethibitisha kuwa China imepokea maombi ya viza kutoka kwa maafisa husika wa Marekani kuhusiana na Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing.

Bw. Zhao Lijian alithibitisha hilo katika mkutano na waandishi wa habari, wakati alipojibu kuhusu ripoti zinazosema serikali ya Marekani imeomba kutuma maafisa 18, hasa wa Wizara ya Mambo ya Nje na ya Ulinzi, kuja China ili kutoa msaada wa kiusalama na matibabu kwa wanariadha wa Marekani, wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing, na baadaye inaweza kuwasilisha maombi ya viza kwa ajili ya maafisa wengine 40.

Msemaji huyo amesisitiza kuwa China itashughulikia ombi la Marekani la kutuma timu ya maafisa wa serikali nchini China na maombi yao ya viza kwa mujibu wa utaratibu wa kimataifa, kanuni husika na kanuni ya usawa.

Bw. Zhao ameongeza kuwa China inataka Marekani kufuata moyo wa Olimpiki kivitendo, kujiepusha kufanya michezo kuwa suala la kisiasa, na kuacha maneno na vitendo potovu vinavyovuruga au kudhoofisha Michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi ya Beijing.