China yatoa kwa mara ya kwanza waraka mweupe kuhusu udhibiti wa uuzaji wa bidhaa nje
2021-12-29 14:44:45| cri

Ofisi ya habari ya Baraza la Serikali la China imetoa waraka mweupe kuhusu udhibiti wa uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, ikiwa ni mara ya kwanza kwa China kutoa waraka mweupe kuhusu udhibiti wa uuzaji wa bidhaa nje.

Waraka huo unalenga kujulisha kwa pande zote msimamo, mfumo na uzoefu wa China katika usimamizi na udhibti wa uuzaji wa bidhaa nje, na kufafanua mapendekezo na hatua za China za kulinda amani na maendeleo ya dunia na usalama wa kitaifa na kimataifa.

Waraka huo umesema, wakati dunia inashuhudia mabadiliko makubwa, hali ya sintofahamu inaongezeka kidhahiri, mfumo na utaratibu wa usalama wa kimataifa umeathiriwa, huku amani ya dunia ikikabiliwa na changamoto na matishio mbalimbali. Hadhi na mchango wa udhibiti wa uuzaji wa bidhaa nje wenye usawa, busara, usio na uonevu katika kukabiliana kwa ufanisi na changamoto na hatari za kikanda na kimataifa, na kulinda amani na maendeleo ya dunia, vinaongezeka siku hadi siku.

Pia waraka huo umeeleza kuwa, nchi mbalimbali duniani zinatilia maanani na kuhimiza kazi za kudhibiti uuzaji wa bidhaa nje, na kuimarisha udhibiti huo kupitia kuzindua na kutekeleza mfumo wa kisheria. China ikiwa mjumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na nchi kubwa zaidi kwa biashara na utengenezaji wa bidhaa duniani, siku zote inafuata kanuni za kulinda usalama wa taifa, amani ya dunia na usalama wa kikanda, na kuboresha udhibiti na usimamizi wa uuzaji wa bidhaa nje.