Tanzania Zanzibar yaahidi kukumbatia teknolojia ya kidijitali ili kuchochea ukuaji wa uchumi
2021-12-30 09:43:52| CRI

Tanzania Zanzibar yaahidi kukumbatia teknolojia ya kidijitali ili kuchochea ukuaji wa uchumi_fororder_Tanzania

Rais wa Tanzania Zanzibar Hussein Ali Mwinyi ameahidi kukumbatia teknolojia ya kidijitali akisema ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi.

Akihutubia kwenye sherehe za mahafali ya 17 ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar rais Mwinyi alisema teknolojia ya kidijitali ni muhimu sana katika dunia ya sasa, hivyo inatakiwa kujiandaa ili kuendana na ulimwengu huu wa ushindani, kwa kuwafanya watoto wawe na elimu ya kompyuta na wawe wahitimu wanaoweza kuajiriwa ili kuharakisha maendeleo. Mwinyi alisema teknolojia ya kidijitali inapaswa kutumika kwa uwezo wake wote katika elimu, na kusisitiza kuwa mamlaka zitaendelea kuwekeza kwenye elimu katika ngazi zote, kwa kupitia upya sera na kuongeza mgao wa bajeti kwenye sekta hiyo ili kuwezesha kuzalisha wataalamu wanaohitajika.

Rais Mwinyi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo hicho, aliahidi kuboresha uendeshaji wa taasisi hiyo ya elimu ya juu na kuiwezesha kutoa wahitimu wenye sifa za juu. Jumla ya wanafunzi 1,894 wa fani mbalimbali, zikiwemo habari, mawasiliano na teknolojia, usimamizi wa fedha, sayansi ya afya na matibabu, utalii na upishi walihitimu kwa mwaka wa masomo 2020/2021.