China na Uganda zatia saini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kiufundi
2022-04-15 09:12:31| CRI

China na Uganda Alhamisi zilitia saini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kiufundi unaolenga kuboresha maisha ya Waganda.

Waziri wa Fedha wa Uganda, Matia Kasaija, alitia saini hati hiyo kwa niaba ya Uganda huku Zhang Lizhong, balozi wa China nchini Uganda akitia saini kwa niaba ya China.

Kasaija alisema makubaliano hayo yatatumika kutekeleza miradi ambayo nchi zote mbili zitakubaliana ili kusaidia mabadiliko ya kijamii na maisha.

Kasaija alisema “kwa miaka mingi, China, bila shaka, imechangia mabadiliko ya kijamii na kiuchumi ya Uganda kupitia ushirikiano katika nyanja nyingi, ambazo ni pamoja na ufadhili wa miradi ya miundombinu kama vile mabwawa ya kuzalisha umeme kwa maji, barabara na maeneo ya kiviwanda, na miradi inayohusu maisha ya watu".

Alibainisha kuwa licha ya athari za janga la COVID-19, China inaendelea kutoa msaada mkubwa wa kifedha nchini Uganda.

Naye Zhang amesema makubaliano hayo ni sehemu ya juhudi zilizotangazwa na China katika Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Baraza la Ushirikiano wa China na Afrika (FOCAC) uliofanyika nchini Senegal mwezi Novemba. Katika mkutano huo, China ilitangaza mipango tisa ya ushirikiano yenye lengo la kukuza ukuaji wa Afrika.