Somalia yaapisha bunge jipya baada ya kuchelewa kwa muda mrefu
2022-04-15 08:58:44| CRI

Wabunge wapya zaidi ya 300 wa Somalia, wakiwemo wa Baraza la Chini 275 na wa Seneti 54 hatimaye waliapishwa Alhamisi katika sherehe iliyofanyika huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, baada ya kuchelewa kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Mwenyekiti wa Tume ya Utekelezaji wa Uchaguzi ya Shirikisho (FEIT) Bw. Muse Gelle Yusuf amesema uchaguzi wa wabunge wengine 25 bado haujafanyika katika majimbo mawili ya shirikisho.

Ameongeza kuwa uchaguzi ulihitimishwa kwa amani licha ya kuongezeka kwa mashambulizi ya kigaidi ya kundi la al-Shabab ambayo yalilenga wajumbe wa uchaguzi, ukosefu wa fedha za kutosha na ukame mkali.

Bunge jipya liliwachagua wabunge wawili wazee, Ali Mohamed Yusuf kama spika wa muda wa Baraza la Juu na Abdisalan Haji Ahmed kama spika wa Baraza la Chini.