Ethiopia yaingiza dola milioni 390 katika miezi 9 iliyopita kutokana na uzalishaji viwandani
2022-04-18 08:42:29| CRI

Wizara ya viwanda ya Ethiopia imesema katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, mauzo ya nje kutokana na sekta ya viwanda ya nchi hiyo yameingiza dola za Kimarekani milioni 390. Shirika la utangazaji la nchi hiyo Fana limesema kiasi hicho ni asilimia 87 ya mapato ya malengo yaliyowekwa kutoka sekta hiyo.

Waziri wa viwanda wa Ethiopia Bw. Melaku Alebel, amesema licha ya ongezeko zuri lililoonekana kwenye ukuaji katika sekta hiyo, bado kuna changamoto kutokana na kukosekana kwa upatikanaji wa mahitaji, changamoto ya miundombinu, kutokuwa na nguvu kazi ya kutosha yenye ujuzi, na fedha.

Mwanzoni mwezi huu wizara ya biashara na mafungamano ya kikanda ya Ethiopia, ilisema nchi hiyo imeingiza dola bilioni 2.52 kutokana na mauzo ya nje katika kipindi cha miezi minane iliyopita.