Katibu mkuu wa UM atoa wito kusitishwa kwa mapigano nchini Ukraine kwa ajili ya misaada ya kibinadamu
2022-04-19 09:16:27| CRI

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres ametoa wito tena kusitishwa kwa mapigano nchini Ukraine ili kuwezesha kutolewa kwa misaada ya kibinadamu ikiwemo usambazaji wa misaada ya kuokoa maisha na uhamishaji wa watu.

Katibu mkuu ametoa wito huo baada ya mashambulizi yanayoendelea kutokea kote nchini Ukraine yakisababisha vifo vingi vya raia na uharibifu mkubwa.

 Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema mazungumzo yenye ufanisi yanahitajika ili kufikia amani ya kudumu kati ya pande zote husika, na UM liko tayari kutoa usaidizi kwa juhudi hizo.

Mratibu wa mambo ya kibinadamu na misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Bw. Martin Griffiths, amewaambia waandishi kuwa kusitishwa kwa mapigano kunaweza kutokea baada ya wiki kadhaa, japo sasa hakuonekani kukaribia.