UM: Raia 35 wameuawa DRC wakati misaada ikicheleweshwa kutokana na hali inayozorota
2022-04-19 09:22:31| CRI

Shirika la haki za kibinadamu la Umoja wa Mataifa limesema raia 35 wameuawa mkoani Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huku likieleza kuwa hali inayozorota imezuia usafirishaji wa misaada.

Ofisi ya uratibu wa mambo ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema, watu 35 wameuawa huko Djugu na Irumu wiki iliyopita, akiwemo mmoja aliyekimbia makazi yake na wengine 19 waliorudi makwao hivi karibuni.

Ofisi hiyo imesema hali ya kukosekana kwa usalama imelazimisha mashirika 9 ya kibinadamu, idara moja ya UM na mashirika manane yasiyo ya kiserikali kusimamisha kwa muda safari zao barabarani huko Irumu na Mambasa, na hivyo kuchelewesha utoaji wa msaada kwa maelfu ya watu.

Hali ya kibinadamu huko Ituri imezidi kuwa mbaya tangu mwezi Oktoba mwaka jana, wakati mashambulizi dhidi ya raia wa kawaida na vituo vya watu waliopotea makazi, yakiongezeka.