Mchango wa wanawake katika kutokomeza malaria duniani
2022-04-19 15:55:45| CRI

Malaria ni ugonjwa wa homa kali unaosababishwa na vimelea vya Plasmodium, ambavyo huenezwa kwa watu kwa kuumwa na mbu jike aina ya Anopheles. Kuna aina 5 za vimelea vinavyosababisha malaria kwa binadamu, na 2 kati ya spishi hizi yaani P. falciparum na P. vivax husababisha tishio kubwa zaidi. P. falciparum ndicho kimelea hatari zaidi cha malaria na vimeenea zaidi katika bara la Afrika. P. vivax ni vimelea vya malaria vinavyotawala katika nchi nyingi nje ya Afrika Kusini mwa Sahara.

Mnamo 2020, karibu nusu ya idadi ya watu ulimwenguni walikuwa katika hatari ya ugonjwa wa malaria. Baadhi ya makundi ya watu ambao wako katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa malaria na kupata ugonjwa mbaya ni watoto wachanga, watoto chini ya umri wa miaka 5, wanawake wajawazito na wagonjwa wenye VVU/UKIMWI, pamoja na watu wenye kinga dhaifu wanaohamia maeneo yenye maambukizi makali ya malaria kama vile wafanyakazi wahamiaji, watu wanaotembea na wasafiri.

Hivyo Siku ya Malaria Duniani ambayo inafanyika Aprili 25 kila mwaka ambayo safari hii itakuwa Jumatatu ijayo ni hafla ya kuangazia mahitaji ya kuendeleza uwekezaji na dhamira endelevu ya kisiasa ya kuzuia na kudhibiti malaria. Siku hii ilianzishwa na nchi wanachama wa WHO katika Mkutano wa Afya Duniani wa mwaka 2007. Hivyo leo katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake tutaangazia ugonjwa huu na mchango wa mwanasayansi wa China mama Tu Youyou aliyegundua dawa ya malaria ya artemisinin.