Mahakama ya Uingereza yaidhinisha Julian Assange kupelekwa Marekani
2022-04-21 09:37:07| CRI

Mahakama ya Westminster ya London imetoa amri ya kuidhinisha rasmi mwanzilishi wa tovuti ya "WikiLeaks" Julian Assange kupelekwa nchini Marekani. Kesi hiyo imekabidhiwa kwa wizara ya mambo ya ndani ya Uingereza, na uamuzi wa mwisho utatolewa na waziri wa mambo ya ndani Bibi Priti Patel.

Bw. Assange mwenye umri wa miaka 50 alianzisha tovuti ya WikiLeaks mwaka 2006, na mwaka 2010 tovuti hiyo ilifichua idadi kubwa ya nyaraka za mawasiliano ya kidiplomasia na hati za siri za jeshi la Marekani wakati wa vita nchini Afghanistan na Iraq. Marekani ilimfungulia mashtaka kwa makosa 18 na mwaka 2019 alikamatwa na kufungwa jela nchini Uingereza. Baadaye, Marekani ilisisitiza Assange kupelekwa Marekani kujibu mashtaka ya kuvujisha hati zinazohusiana na siri za Marekani na kuhatarisha maisha ya watu.