Umoja wa Mataifa wachunguza operesheni ya kijeshi ya Mali iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 200
2022-04-21 09:32:28| CRI

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema uchunguzi dhidi ya operesheni ya kijeshi nchini Mali inayodaiwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya 200 umezuiwa na maofisa wa nchi hiyo.

Bw. Dujarric amesema operesheni hiyo iliyofanywa na jeshi la Mali wiki tatu zilizopita likiambatana na wanajeshi wa kigeni, linadaiwa kutekeleza mauaji na vitendo vingine vya kukiuka haki za kibinadamu katika kijiji cha Moura nchini humo. Japo jeshi la Mali lilidai kuwa operesheni hiyo ilikuwa dhidi ya kundi la kigaidi, habari kutoka Ofisi ya Mambo ya Haki za Kibinadamu imeonyesha wahanga wengi walikuwa ni raia wa kawaida.

Wajumbe wa haki za kibinadamu wa UM wamesema serikali ya mpito wa Mali imeanzisha uchunguzi dhidi ya operesheni hiyo. Bw. Dujarric ametoa wito kwa serikali hiyo kuhakikisha uchunguzi unafanyika kwa wakati, kwa ukamilifu, bila upendeleo, na pia kuhakikisha wachunguzi wa UM wanafika salama kwenye eneo husika bila kizuizi.