Emmanuel Macron ashinda duru ya pili ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa
2022-04-25 14:01:27| CRI

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameshinda kwenye duru ya pili ya uchaguzi wa urais wa Ufaransa kwa kupata asilimia 58 ya kura. Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa jana jioni na televisheni ya Ufaransa BFMTV, mshindani wa Bw. Macron, ambaye ni mgombea wa mrengo mkali wa kulia Bibi Marine Le Pen, amepata asilimia 42 ya kura.

Katika hotuba yake baada ya kupata matokeo ya awali, Bibi Le Pen amesema matokeo yenyewe ni ushindi wa kishindo, kwani mamilioni ya watu wameipigia kura kambi ya utaifa na mabadiliko.

Amewashukuru hasa wafuasi wake kutoka maeneo ya vijijini na wale wa maeneo ya ng'ambo waliomwezesha kuongoza wakati wa uchaguzi.

Ikiwa ni mara ya pili ya uchaguzi wa urais kushindwa mbele ya Bw. Macron, Bibi Le Pen ametoa wito kwa wafaransa kumpigia kura katika uchaguzi ujao wa wabunge.

Mwaka wa 2017, Bw. Macron na Bibi Le Pen pia waligombea urais wa Ufaransa katika duru ya pili, Bw. Macron alichaguliwa kwa kupata asilimia 66.1 ya kura.