Walimu watatu wa China wafariki dunia kufuatia basi la Taasisi ya Confucious kushambuliwa Karachi
2022-04-27 10:57:51| CRI

Walimu watatu wa China walifariki dunia na mwingine mmoja kujeruhiwa baada ya mlipuaji wa kujitoa muhanga kujilipua karibu na basi walilokuwa wakisafiria la Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Karachi, kusini mwa Pakistan jana Aprili 26.

Akizungumzia tukio hilo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema kuwa China inalaani vikali shambulizi hilo la kigaidi na kutoa salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa, na kuitaka Pakistan ifanye uchunguzi kamili ili kuwafikisha wahusika mbele ya sheria. Pia ameitaka Pakistan kuchukua hatua madhubuti kulinda usalama wa raia wa China nchini humo na kuzuia tukio kama hilo lisije kutokea tena.

Waziri mkuu wa Pakistan Shahbaz Sharif siku hiyo alikwenda katika ubalozi wa China nchini humo kutoa salamu za rambirambi kutokana na vifo vya raia wa China kwenye tukio hilo, na kusema kuwa serikali ya Pakistan itachunguza tukio hilo kikamilifu na kutoa adhabu kali kwa wahusika, pia ameahidi kuimarisha hatua za kuhakikisha usalama wa raia wa China nchini Pakistan, na kutoruhusu kundi lolote kuharibu urafiki kati ya nchi hizo mbili.

Bw. Sharif amesisitiza kuwa Pakistan inapinga aina zote za ugaidi, na kwamba njama ovu za maadui wa uhusiano wa wenzi wa kimkakati kati ya Pakistan na China hazitavuruga undugu uliopo kati ya nchi hizo mbili, na wala hazitaathiri ushirikiano kati yao.