Wanasayansi wa Afrika wasema siku za mbele za kijani ziko hatarini kutokana na ukataji wa miti
2022-05-04 10:47:28| CRI

Kupotea kwa eneo la misitu katika Afrika kunakochangiwa na athari za hali ya hewa, matumizi mabaya ya ardhi na ukuaji wa miji kunaweza kupunguza kasi ya mageuzi ya Afrika kuelekea siku za mbele za kijani na imara.

Wakiongea kwenye kongamano kwa njia ya video huko Nairobi Kenya sambamba na Mkutano wa 15 wa Misitu Duniani ulianza tarehe 2 Mei na kuendelea hadi tarehe 6 Mei huko Seoul, Korea Kusini, wanasayansi wametoa wito wa kuimarisha ulinzi wa misitu ya Kitropikali ya Afrika ili kuongeza nguvu shughuli za kukabiliana na hali ya hewa.

Godwin Kowero, katibu mtendaji wa Baraza la Misitu la Afrika lenye makao yake mjini Nairobi, amesema ukataji miti unaohusishwa na kushindwa kwa uongozi, shughuli mbaya za kilimo na utekelezaji mbaya wa sheria ni tishio kwa ajenda ya kijani ya Afrika.

Naye Djibri Dayamba, afisa mwandamizi wa programu katika Baraza la Misitu la Afrika, amesema eneo la misitu la Afrika linalokadiriwa kuwa hekta milioni 636,639 au asilimia 16 ya eneo lote duniani, linapaswa kutumika kiuendelevu ili kuendeleza ajenda endelevu. Amezitaka nchi za Afrika kuhimiza mifumo ya chakula inayopatana na maumbile na kuwekeza katika nishati safi na utalii wa kimazingira ili kuimarisha uhifadhi wa mandhari ya misitu.