AU na IGAD walaani shambulizi la kigaidi dhidi ya vikosi vya ATMIS
2022-05-05 10:33:43| CRI

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Mousa Faki Mahamat amelaani vikali shambulizi la kigaidi lililofanywa na wanamgambo wa al-Shabaab dhidi ya kambi ya Tume ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS). Kwenye taarifa iliyotolewa Jumanne jioni na Tume hiyo, Bw. Mahamat ametoa mkono wa pole kwa familia ya walinda amani wa Burundi waliopoteza maisha yao wakisaidia kuleta amani na utulivu nchini Somalia na kuitaka jamii ya kimataifa kuzidi kuiunga mkono serikali ya Somalia na watu wake ili kufikia amani na usalama wa kudumu.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa IGAD Wokneh Gebeyehu ametoa rambirambi zake kwa familia za walinda amani, serikali, watu wa Burundi na Somalia, na kusema IGAD ina uhakika kwamba mashambulizi haya hayatazuia wala kubadilisha nia ya IGAD na washirika wa kimataifa katika kuunga mkono watu wa Somalia wakati wakitafuta amani na utulivu wa kudumu.

Burundi imetangaza kuwa walinda amani wake 10 wameuawa na wengine watano hawajulikani walipo kwenye shambulizi lililofanywa mapema Jumanne na al-Shabaab katika kituo cha askari wa Burundi huko Baraf, mkoa wa Shabelle nchini Somalia. Askari 25 pia wamejeruhiwa kwenye shambulizi hilo.