Watu zaidi ya 1,000 wafariki dunia katika ajali za barabarani nchini Tanzania katika muda wa miezi tisa
2022-05-06 10:19:08| CRI

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Hamad Yussuf Masauni amesema kuwa takriban watu 1,191 walifariki dunia na 2,139 kujeruhiwa kutokana na ajali za barabarani 1,594 zilizotokea nchini humo kati ya mwezi Julai mwaka 2021 na mwezi Machi mwaka 2022.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu kumekuwa na ongezeko la ajali za barabarani 366, vikipanda kwa asilimia 29.8. Amesema ajali nyingi zinasababishwa na uzembe wa madereva, ubovu wa magari na ubovu wa barabara.

Aidha amebainisha kuwa polisi waliwafutia leseni madereva 87 na kuwafungia leseni kwa muda tofauti madereva 141 ikiwa ni adhabu baada ya kuhusishwa na ajali za barabarani.