Jumapili ya tarehe 8 ilikuwa ni siku ya mama duniani, siku hii inasherehekewa ili kuonyesha heshima na thamani ya mama katika familia na kuthamini mchango na ushawishi wao mkubwa katika jamii. Na itakapofika Juni 21 kina baba nao hawatakuwa nyuma kwani watasherehekea siku yao kama ilivyoadhimishwa kwa kina mama. Siku hizi mbili kwa familia iliyokamilika yaani yenye baba na mama ina thamani kubwa sana. Kwani watoto kwa nyakati tofauti wanapata fursa ya kushukuru mchango na malezi ya mama na vilevile kushukuru malezi na mchango wa baba katika familia. Lakini kuna kundi lile la watoto ambao familia yao haijakamilika, ni aidha anaishi na mama au baba pekee. Tunafahamu kuwa watoto wanaopitia malezi ya mzazi mmoja huwa wanakuwa na changamoto nyingi sana. Hivyo leo hii kwenye kipindi cha Ukumbi wa wanawake tutaangalia kati ya mzazi mwanamke yaani mama anayelea watoto pekee na mzazi mwanaume yaani baba anayelea watoto pekee ni nani anakabiliwa na changamoto nyingi zaidi. Ingawa kipindi hiki kinahusu wanawake lakini leo hii tumeonelea tuangalie changamoto zinazokumba pande zote mbili za mama au baba asiye na mwenza.