Watu milioni 18 waathiriwa na ukame Afrika Mashariki
2022-05-17 09:57:13| CRI

Zaidi ya watu milioni 18 nchini Ethiopia, Somalia na Kenya zilizoko kaskazini-mashariki mwa Afrika wameathiriwa vibaya na ukame, na kati yao, watu milioni 16.7 wanakabiliwa na ukosefu wa chakula.

Hayo yamesemwa na msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric. Amesema idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka katika wiki zijazo, na kuongeza kuwa Pembe ya Afrika inakabiliwa na ukame utakaoendelea kwa muda mrefu zaidi katika miongo minne iliyopita.

Dujarric amesema, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mambo ya kibinadamu na mratibu wa Misaada ya Dharura Martin Griffiths, alishuhudia athari mbaya ya upungufu wa mvua katika msimu wa nne mfululizo wa mvua katika eneo hilo wakati wa ziara yake nchini Kenya.

Dujarric amesema, Griffiths pia alikutana na maafisa wa Kenya na kujadiliana nao kuhusu hatua za serikali katika kukabiliana na ukame, na haja ya utoaji msaada wa dharura kwa jamii zilizoathiriwa na ukame. Griffiths alionya kwamba kama msaada mpya hautatolewa mara moja, eneo hilo litakabiliwa na hasara kubwa ya maisha.