Takwimu za uchumi kwa mwezi Aprili nchini China zimeshuka kutokana na athari za Omicron, sera zaidi za kuunga mkono uchumi zahimizwa
2022-05-17 14:22:06| cri

Uzalishaji wa viwanda kwa mwezi Aprili nchini China ulipungua kwa asilimia 2.9 ikilinganishwa na mwaka jana, huku mauzo ya rejareja yakipungua kwa asilimia 11.1, na kuonyesha kuwa athari za virusi vya Omicron zimezorotesha uchumi. Hata hivyo, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya China (NBS) imesema kwa mwezi Mei kuna dalili za kuimarika kwa uchumi na ukuaji katika robo ya pili unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu.

Wachambuzi wanaona kadri hali ya ufufukaji itakavyoongezeka katika mwezi Juni, robo ya pili huenda ikashuhudia uchumi ukikua kwa asilimia 4.8, kiwango sawa na cha robo ya kwanza, na kutandika njia kufikia lengo la ukuaji wa kila mwaka la karibu asilimia 5.5.

NBS imesema mwezi April uzalishaji viwandani ulipungua kwa asilimia 2.9, kutoka ukuaji wa asilimia 5 ya mwezi Machi, na mauzo ya rejareja yalipungua kwa zaidi ya asilimia 11. Takwimu zote mbili zilikuwa chini kuliko matarajio ya soko, zinaonyesha madhara ya janga la Omicron kwenye uchumi.

Hata hivyo uwekezaji wa mali zisizohamishika ulishuhudia ongezeko la asilimia 6.8 na kufikia yuan trilioni 15.4 ($2.27 trilioni), lakini limepungua kwa asilimia 2.5 ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka huu kutokana na athari za Omicron.