Ukuaji wa uchumi wa dunia wapungua kutokana na mgogoro wa Ukraine
2022-05-19 08:33:27| CRI

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Umoja wa Mataifa kuhusu Hali na Matarajio ya Uchumi wa Dunia (WESP) imesema, uchumi wa dunia unatarajiwa kukua kwa asilimia 3.1 mwaka huu, ikiwa ni chini ya asilimia 4.0 iliyokadiriwa mwezi Januari, sababu kuu ikiwa ni operesheni maalum ya kijeshi ya Russia nchini Ukraine.

Kama matarajio ya katikati ya mwaka yanavyoonyesha, mgogoro huo umevuruga ufufukaji wa uchumi kutokana na janga la COVID-19, na kusababisha mgogoro wa kibinadamu barani Ulaya, kuongezeka kwa bei ya chakula na bidhaa, na kuzidisha shinikizo la kupanda kwa gharama za maisha.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, vita ya Ukraine inasababisha mgogoro ambao unaathiri soko la nishati duniani, kuvuruga mfumo wa kifedha na kuongeza matishio zaidi kwa nchi zinazoendelea.