Wanaharakati wa Afrika wataka miji ya kijani barani humo ili kuongeza unyumbufu
2022-05-20 08:35:34| CRI

Wanaharakati wanaohudhuria mkutano wa Miji ya Afrika unaofanyika mjini Kisumu nchini Kenya wamesema, kuna haja ya kuongeza kasi ya mageuzi ya kijani na unyumbufu kwa ajili ya miji ya Afrika, vinavyoahidi ustawi wa pamoja, jumuishi na matokeo mazuri ya kiafya kwa wakazi.

Kaimu mkurugenzi wa Jumuiya ya Haki ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Afrika (PACJA) Charles Mwangi amesema, kuna haja ya miji ya Afrika kujadiliana kuhusu muundo unaoweza kuboresha unyumbufu wao kuendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Mkurugenzi wa Idara ya Hali ya Hewa katika Muungano wa Miji na Serikali za Mitaa za Afrika, Mohamed Nbou amesema, mabadiliko ya tabianchi ni tishio kwa kutimiza lengo la mwaka 2030 la dunia katika miji ya bara hilo kutokana na majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa yaliyozidisha umasikini, magonjwa na ukosefu wa usawa.