Waziri wa Mambo ya Nje: “Mkakati wa Indo Pasifiki” wa Marekani utashindwa tu
2022-05-23 08:43:57| CRI


Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema mpango wa Marekani uitwao “Mkakati wa Indo Pasifiki” utashindwa tu, kwani unasababisha jumuiya ya kimataifa kuwa na wasiwasi mkubwa na kuwa macho, hasa katika eneo la Asia-Pasifiki.

Bw. Wang ameyasema hayo kwa wanahabari baada ya mkutano wake na mwenzake wa Pakistan Bilawal Bhutto Zardari ambaye yupo ziarani huko Guangzhou. Amebainisha kuwa mkakati huo umeondoka kwenye dhamira yake, na sasa sio tu unajaribu kufuta jina la “Asia-Pasifiki” na ufanisi mzuri wa ushirikiano wa kikanda, bali pia unajaribu kufuta mafanikio na kasi ya maendeleo ya amani yaliyotokana na juhudi za pamoja za nchi za eneo hilo katika miongo iliyopita.

Wang pia amesema watu wa Asia-Pasifiki hadi leo wanakumbuka migogoro na makabiliano yaliyosababishwa na ukandamizaji, na wanataka utulivu wa kitaifa na maisha ya furaha, huku nchi za ndani ya eneo hilo zikiweza kuishi pamoja kwa masikilizano na kutafuta ushirikiano wa kunufaishana.