Tanzania yatangaza kuchukua hatua za kudhibiti wanyama pori wanaopotea njia
2022-05-25 10:33:23| CRI

Mamlaka za Tanzania zimetangaza kuchukua hatua za muda mrefu na mfupi zinazolenga kudhibiti wanyama pori wanaopotea njia kutoka kwenye maeneo yao wanayohifadhiwa na kufanya uharibifu kwenye vijiji.

Kwenye taarifa yake Waziri wa Maliasili na Utalii Pindi Chana amesema wanyama hao wakiwemo tembo, simba na viboko wanaripotiwa kuvamia vijiji katika wilaya takriban 53 kati ya 134. Amebainisha kuwa hatua ya muda mfupi ni pamoja na kuanzisha vituo 11 vitakavyotumiwa na walinzi ili kusaidia kudhibiti wanyama pori wanaopotea na kutoa namba ya simu kwa ajili ya kuripoti wanyama hao. Kwa upande wa hatua ya muda mrefu waziri Chana ametaja ni pamoja na kununua helikopta kwa ajili ya kufanya doria angani na kuimarisha doria ya ardhini kwa walinzi wa wanyama.

Taarifa hiyo imesema sababu ya wanyama hawa kupotea ni mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanasababisha kukauka kwa vyanzo vya maji na wakati mwingine ni mafuriko.