Idadi ya watalii wa Kenya yavuka asilimia 85 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022
2022-05-25 10:30:38| CRI

Kulingana na takwimu mpya za kiuchumi kutoka Ofisi ya Takwimu ya Kitaifa ya Kenya (KNBS), idadi ya watalii waliofika Kenya imevuka asilimia 85 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022 huku hali ikirejea kama kawaida katika sekta hiyo baada ya kukatizwa na COVID-19.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa Kenya imepokea watalii 225,331 kupitia uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Moi katika mji wa pwani wa Mombasa, wakilinganishwa na 121,739 katika kipindi kama hicho mwaka wa 2021.

Kuongezeka kwa idadi ya watalii waliowasili kunaonyesha kufufuka kwa sekta ya utalii ambayo iliathirika vibaya na janga la COVID-19, wakati ambapo chanjo nchini na duniani kote zikiendelea kuimarishwa.