Mkuu wa UNICEF ataka kuchukuliwa hatua za kuwalinda watoto baada ya shambulio la risasi katika shule ya Texas Marekani
2022-05-26 10:55:00| CRI

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) Bi. Catherine Russell amehoji kuwa ni watoto wangapi wanapaswa kufa kabla ya viongozi kuchukua hatua ya kuwaweka salama watoto pamoja na shule.

Akitolea mfano wa vifo vilivyotokea katika shambulizi la risasi lililofanyika katika shule ya msingi ya Texas nchini Marekani, Bi. Catherine Russell amesema watoto hao walivamiwa na kuuawa huko Uvalde, Texas, wakati wapo shuleni, sehemu moja iliyo nje ya nyumbani kwao ambapo wanapaswa kuwa salama zaidi.

Ameongeza kuwa tukio hilo limesababisha vifo vya watoto 19, mwalimu na mfanyakazi wa shule, na wengine wengi walioshuhudia mauaji hayo watakuwa na makovu ya kihisia na kisaikolojia kwa maisha yao yote.