Siku ya Fistula Duniani
2022-05-27 07:43:33| CRI

Tarehe 23 Mei ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Fistula ya Uzazi. Fistula ni tatizo la kuwepo na tundu katika njia ya uzazi linalotokana na mwanamke mjamzito kuwa na uchungu kwa muda mrefu bila ya kupata huduma, kama vile upasuaji. Fistula pia inaweza kusababishwa na mimba za utotoni, ukeketaji, na ajali. Mwaka 2003, Mfuko wa Idadi ya Watu wa Umoja wa Mataifa (UNFPA) na wenza wake lilizindua kampeni ya dunia nzima ya kumaliza tatizo la Fistula, ushirikiano wa pamoja ili kuzuia Fistula na kurejesha afya kwa walioathiriwa na tatizo hilo. Mwaka 2012, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa tarehe 23 Mei ya kila mwaka itakuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kumaliza Fistula ya Uzazi, Siku ambayo ilianza kuadhimishwa mwaka 2013. 

Mwaka huu, kaulimbiu ya Siku hiyo ni “Tokomeza Fistula: Imarisha Huduma za Afya, Wezesha Jamii!” Tatizo la Fistula sio tu ni suala la afya ya jamii, bali pia ni suala la haki za binadamu, ambayo inahusiana na kila mtu kuwa na haki ya afya bora na maisha yenye heshima. Hii inatokana na wanawake wanaosumbuliwa na tatizo la Fistula kutengwa na jamii, na kuonekana kama wana mkosi. Wanawake wengi wanaosumbuliwa na tatizo hili wamejikuta wakikabiliwa na maisha magumu, na mwishowe huwa wanajitenga na jamii. Katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake leo hii tutaangalia tatizo la hili la Fistula kwa wanawake, na hatua zinazochukuliwa kukabiliana nalo.