Putin asema nchi za magharibi zikiondoa vikwazo Russia itauza nje chakula na mbolea
2022-05-27 09:20:51| CRI

Rais Putin wa Russia jana alisema Russia inapanga kuuza nje chakula na mbolea ili kutoa mchango katika kukabiliana na msukosuko wa chakula duniani, lakini sharti lake ni kuwa nchi za magharibi zitaondoa vikwazo vilivyowekwa kutokana na madhumuni ya kisiasa.

Habari kutoka tovuti ya Ikulu ya Russia imesema Putin ameongea kwa njia ya simu na waziri mkuu wa Italia Bw. Mario Draghi, na kujadiliana masuala ya hali ya Ukraine na usalama wa chakula duniani. Putin amesema hakuna msingi wowote katika kuishutumu Russia juu ya suala la utoaji wa mazao ya kilimo kwenye soko la dunia. Changamoto ya sasa inahusiana na kutokuwepo utaratibu kwenye sekta mbalimbali na mnyororo wa ugavi duniani, pamoja na sera za fedha za nchi za magharibi kwenye kipindi cha janga la Corona.

Putin ameongeza kuwa Russia imechukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa usafiri baharini, lakini kazi hizo zinazuiliwa na upande wa Ukraine.