China na Tanzania zasaini mpango mpya wa utekelezaji wa makubaliano ya kiutamaduni
2022-05-27 09:15:26| CRI

Serikali za China na Tanzania jana Alhamis zilisaini mpango mpya wa 2022-2025 wa utekelezaji wa makubaliano ya kiutamaduni unaolenga kuimarisha ushirikiano wa pande mbili kwenye nyanja mbalimbali.

Kwa mujibu wa ubalozi wa China nchini Tanzania, mpango huo uliosainiwa jijini Dar es Salaam na balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjiang na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa ambao unaangazia maeneo ya utamaduni, Sanaa, utalii, uandishi wa habari, michezo na elimu, unadhamiria kuimarisha kwa kina urafiki wa jadi kati ya nchi mbili. Mpango huo pia unahamasisha ushiriki mpana katika kukuza utalii na kutumia bidhaa za utamaduni na utalii kwa pamoja kati ya pande mbili.

Akiongea baada ya kusainiwa, Mchengerwa amesema ushirikiano wa kiutamaduni kati ya China na Tanzania unailetea tija nyingi Tanzania. Naye balozi Chen amesema nchi hizi mbili zinafurahia urafiki mkubwa wa jadi na zimekuwa zikishirikiana kwa karibu kwenye maeneo ya utamaduni, Sanaa, redio, filamu, televisheni, elimu na sayansi na teknolojia.