Wafanyabiashara wanane wakamatwa Tanzania kutokana na kusafirisha dhahabu kwa magendo
2022-05-30 10:04:21| CRI

Waziri wa madini wa Tanzania Bw. Dotto Biteko amesema watu wanane wamekutwa katika mkoa wa Geita wakisafirisha kwa magendo nje ya nchi kiasi cha dhahabu kisichojulikana.

Akiongea na wachimbaji wadogo katika eneo la Lwamgasa, Bw. Biteko amesema serikali imeanzisha msako wa wafanyabiashara wa dhahabu wasio waaminifu, baada ya mauzo ya dhahabu katika vituo vya mauzo kuanza kupungua.

Bw. Biteko amewataka wafanyabiashara hao kuacha kununua dhahabu mitaani na badala yake wanunue kutoka kwenye vituo vya madini vinavyoendeshwa na serikali.

Mwaka 2019 Tanzania ilianzisha vituo vya ununuzi wa dhahabu vinavyosimamiwa na serikali, kwa lengo la kupunguza usafirishaji nje kiharamu wa dhahabu na madini mengine.