Serikali ya Afrika Kusini yaazimia kuwezesha uchumi wa watu weusi
2022-05-31 09:01:59| CRI


Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema mageuzi na ukuaji wa kiuchumi nchini vitategemea kuondoa mzunguko wa maendeleo duni kupitia uwezeshaji wa kiuchumi na ujasiriamali wa watu weusi kwani vitu hivi vimeungana, na hakiwezi kuwepo kimoja bila kingine.

Amesisitiza kuwa kuwezesha uchumi wa watu weusi ni sehemu muhimu ya mpango wa serikali wa kujenga upya na kufufua uchumi wakati nchi ikiendelea kufufuka kutokana na janga la UVIKO-19.

Ramaphosa amesema mwaka jana serikali iliidhinisha randi bilioni 2.5 sawa na dola za kimarekani milioni 161.6 katika kuunga mkono tena viwanda vya watu weusi kwa njia ya mkopo kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Viwanda na Uwezeshaji wa Kitaifa, pamoja na kutoa ruzuku kutoka Idara ya Biashara na Viwanda (DTIC), ambao ni mpango wa uhamasishaji ili kuunda zama mpya ya viwanda vya watu weusi.

Mwaka 2003, serikali ya Afrika Kusini ilianzisha sheria ya Uwezeshaji Mpana wa Watu Weusi Kiuchumi (BBBEE) ili kubadili na kurekebisha mpango wa uchumi wa ubaguzi wa rangi ambao uliwatenga watu wengi weusi. Mpango huo ulichangia kurekebisha hali ya kutokuwepo kwa usawa na kuhakikisha ushiriki wa maana kwenye uchumi miongoni mwa watu wengi.