Hatua ya Sudan ya kuondoa hali ya dharura ya kitaifa yapongezwa
2022-05-31 08:59:32| CRI

Uamuzi wa Mwenyekiti wa Baraza la mamlaka ya Mpito la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan wa kuondoa hali ya dharura ya kitaifa na kuwaachilia wafungwa wa kisiasa umepokelewa kwa furaha wakati nchi hiyo inakabiliwa na msukosuko wa kisiasa kwa miezi kadhaa.

Utaratibu wa pande tatu wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Shirika la Maendeleo la Kiserikali la Nchi za Afrika Mashariki IGAD Jumatatu ulikaribisha uamuzi huo "kama hatua chanya za kuandaa mazingira yanayohitajika kufikia suluhu ya kutatua msukosuko wa sasa wa kisiasa kwa amani."

Katika taarifa yao, pande hizo tatu zimehimiza wadau wote kuwa tayari kwa mazungumzo ya kiujenzi kwa nia njema juu ya suluhisho la kisiasa na njia ya amani ya kuondoa mzozo uliopo.

Chama cha Taifa cha Umma nchini Sudan, ambacho ni chama kikuu katika Muungano wa Upinzani wa Uhuru na Mabadiliko, pia kiliona kuondolewa hali ya dharura kama hatua nzuri.