WHO yaonya kutokea kwa maambukizi mengi zaidi ya monkeypox wakati wa majira ya joto
2022-06-01 08:53:23| CRI

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kwamba linalenga kudhibiti mlipuko wa monkeypox kwa kuzuia maambukizi kwa binadamu katika kiwango cha juu kiwezekanacho, na kuonya kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kutokea maambukizi mengi zaidi barani Ulaya na kwengineko.

Kwenye taarifa yake WHO imesema bara la Ulaya bado ni kitovu na eneo linalosambaa zaidi mlipuko wa ugonjwa huo, ambao pia umeripotiwa maeneo mengine ya nje yakiwemo Afrika magharibi na kati.

Akijibu kuhusu kuongezeka kwa kesi za ugonjwa wa monkeypox Ulaya nzima katika wiki mbili zilizopita, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Hans Kluge ametaja hatua zinazohitajika kuchukuliwa zikiwemo kuchunguza na kudhibiti haraka hali hii inayokua kwa kasi.

Ofisi ya WHO barani Ulaya ina wasiwasi kwamba hatua ya hivi karibuni ya kuondoa zuio kwa wasafiri wa kimataifa inaweza kuchangia kasi ya maambukizi.