Mchango wa wanawake katika ulinzi wa mazingira
2022-06-06 08:00:00| CRI

Suala la mabadiliko ya tabianchi limekuwa na litaendelea kuwa na madhara makubwa na ya kudumu kwa mazingira, maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Wanawake wanazidi kuonekana kama watu walio kwenye hatari kubwa zaidi ya kuathirika na mabadiliko ya tabianchi kuliko wanaume, kwani wengi wao ndio masikini duniani na wanategemea zaidi maliasili ambazo kwa sasa zimekuwa kwenye hatari kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Mabadiliko haya ya tabia nchi yanatokana na shughuli mbalimbali za kizembe zinazofanywa na watu duniani. Mwanamke akibeba nafasi yake kama mwalimu na mlezi kwenye jamii, anajitahidi sana kuhakikisha mazingira yanalindwa na kuwa salama ili kuepukana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Umoja wa Mataifa kwa upande wake pia unatambua juhudi na mchango wa wanawake na wasichana duniani kote. Wanawake hawa wanaongoza katika kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ili kujenga mustakabali endelevu zaidi kwa wote. Hivyo katika kipindi cha leo cha Ukumbi wa Wanawake tutaangalia juhudi za uhamasishaji zinazofanywa na wanawake katika suala la ulinzi wa mazingira.