Rais wa Zanzibar aishukuru China kwa msaada katika sekta ya afya
2022-06-08 08:53:24| CRI

Rais Hussein Ali Mwinyi wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ameishukuru China kwa kutoa msaada katika sekta ya afya.

Rais Mwinyi ametoa shukurani zake kwa Serikali ya China alipokutana na timu ya madaktari wa China kutoka mkoa wa Jiangsu mashariki mwa China ambao wanatoa huduma za matibabu katika hospitali za Zanzibar. Amesema madaktari wa China wanaofanya kazi Zanzibar wamesaidia kukabiliana na upungufu wa madaktari bingwa, na kuwashukuru madaktari hao kwa kutoa ujuzi wao wa matibabu kwa madaktari wa ndani.

China kwa muda mrefu imekuwa ikiiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya kupitia utoaji wa dawa, vifaa tiba na madaktari bingwa.