Rais wa China ajibu barua ya wanafunzi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere
2022-06-10 08:42:19| CRI

Rais Xi Jinping wa China Jumatano wiki hii amejibu barua aliyotumiwa na  wanafunzi waliohitimu Semina ya Makada Vijana wa Vyama Sita vya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika kwenye Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere nchini Tanzania. 

Kwenye barua hiyo, rais Xi amesema, anafurahia mafanikio ya semina hiyo, ambapo wanafunzi walijifunza na kupata maendeleo ya pamoja kuhusu masuala ya malengo gani ya maendeleo ambayo vyama tawala vinavyoongoza nchi yao  yanatakiwa kufikiwa katika zama mpya, na namna ya kutimiza maendeleo hayo.

Rais Xi amesema, wanafunzi wa semina hiyo walikaza nia ya kuwa watangulizi wa zama hizi, na mhimili wa ustawi wa taifa, na hilo ndilo lengo la kujengwa kwa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere. Pia aliwatia moyo wanafunzi hao wachangie mchakato wa kutimiza ustawi wa taifa na ufufukaji wa Afrika.

Rais Xi amewataka wanafunzi hao kujikita katika mambo ya urafiki kati ya China na Afrika, na kuenzi moyo wa ushirikiano wa kirafiki kati ya pande hizo mbili, ili kuchangia ujenzi wa kiwango cha juu wa Jumuiya ya China na Afrika yenye mustakabali wa pamoja .